UMUHIMU WA RASILIMALI WATU
UMUHIMU WA RASILIMALI WATU
Na: YAHYA JUMA MAFULA
Singida, Tanzania.
Watu ni rasilimali muhimu kwa ukuaji wa taasisi na taifa lote kwa ujumla. Kuwa na rasilimali fedha, rasilimali ngumu, rasilimali asili, rasilimali teknolojia ama rasilimali muda pekee hakuwezi kuleta maendeleo yanayotarajiwa pasipokua na rasilimali watu. Rasilimali watu ndio hutumia rasilimali nyingine kuwezesha ufikiaji wa malengo. Kwa lugha nyingine rasilimali watu huitwa wafanyakazi ama watumishi.
Rasilimali watu ni nini?
Hawa ni watu wanaofanya kazi kwa mwajiri husika, kwa makubaliano ya kulipwa ujira kwa jitihada zao katika kutimiza malengo ya kundi, taasisi ama taifa.
Aina za Rasilimali watu
Aina za wafanyakazi hutegemena na mikataba husika ambayo hao wafanyakazi huajiriwa nayo. Mikataba ya wafanyakazi hao ni kama ifuatavyo;
(a) Wafanyakazi wa mikataba ya kudumu
Hawa ni wafanyakazi wanaoajiriwa kwa masharti ya moja kwa moja, kwamba wataitumikia taasisi mpaka watakapofikia umri wao wa kustaafu. Kwa mujibu wa sheria za Tanzania, mtumishi wa umma atastaafu pindi atakapofikisha umri wa miaka 60, ama kwa hiari yake akifikisha miaka 55.
(b) Wafanyakazi wa mikataba ya muda mfupi
Hawa ni wafanyakazi wanaoajiriwa kwa makubaliano ya kufanya kazi katika taasisi kwa muda husika, na ajira yao humalizika pindi muda huo unapokamilika. Mfano, miaka mitatu, minne ama vinginevyo.
(c) Wafanyakazi wa mikataba ya kazi husika
Hawa ni wafanyakazi wanaoingia makubaliano ya kufanya kazi fulani katika taasisi, jamii ama taifa. Pindi wafanyakazi hawa wanapokamilisha kazi waliyopewa, ajira yao hufikia ukomo. Mfano, wakandarasi wa majengo ama barabara.
Nini faida za Rasilimaliwatu?
Kama kiini cha maendeleo, wafanyakazi wana faida nyingi kuliko watu wengi wanavyodhani. Faida hizi zinaonesha wazi kwamba wafanyakazi ndiyo kiini cha maendeleo ya jamii na taifa lolote hapa duniani. Tuzitizame faida kuu nne za Rasilimali watu;
(a) Kuitunza familia
Hali halisi ya Tanzania inaonesha kwamba wafanyakazi wengi ndio hutegemewa na ndugu na familia zao. Kila mfanyakazi ana wastani wa watu 4-5 wanaomtegemea kiuchumi. Wafanyakazi hawa hutumia mishahara yao kuendesha maisha yao na ndugu zao. Hivyo kupitia mishahara yao wafanyakazi hawa huwatunza, kuwasomesha na kuwaendeleza ndugu na jamaa zao wa karibu.
(b) Kulitumikia taifa
Kupitia utekelezaji wa wajibu na majukumu yao, wafanyakazi hawa hulitumikia taifa kwa kuleta maendeleo mbali mbali nchini. Mipango mbalimbali ya kimaendeleo katika taifa huwategemea wafanyakazi ili kufanyika kwake.
(c) Kuchangia mapato ya taifa
Kupitia kodi ya moja kwa moja inayokatwa katika mishahara ya watumishi, serikali hukusanya kiasi kikubwa cha mapato. Mapato haya ndio yanayotumika kufanya utekelezaji wa miradi ya kimaendeleo katika taifa.
(d) Kuhudumia wananchi
Pia wafanyakazi hutoa huduma mbali mbali kwa wananchi na kutatua kero na mahitaji yao. Kwakua taasisi mbalimbali za kiserikali zimewekwa kwa lengo la kuhudumia wananchi, ni wafanyakazi ndio wanaohusika na utoaji wa huduma hizo. Mfano, hospitalini, mashuleni na kwingineko.
Ahsante!
Wasiliana nami;
Kupitia simu, sms ama WhatsApp kupitia nambari +255 744 015 186
Email: jumay5154@gmail.com
Instagram na Twitter: Yahya Juma Mafula
Comments
Post a Comment